
Falcao
UNAWAKUMBUKA Andriy Shevchenko na Fernando Torres? Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho ameombwa awakumbuke mastaa hao wawili, kabla hajafikiria mara mbili kumchukua mshambuliaji wa Monaco, Radamel Falcao.
Mwandishi maarufu wa michezo wa Gazeti laDaily Mail la Uingereza, Rik Sharma ana hofu kwamba Falcao ataishia kuchemsha Stamford Bridge kama ilivyo kwa Shevchenko na Torres.
Staa huyo juzi alishindwa kuibeba Colombia katika pambano la Copa Amerika dhidi ya Venezuela na kukubali kichapo cha bao 1-0 na Sharma anaamini kuwa licha ya Mourinho kujigamba kuwa atamrudisha Falcao halisi lakini kuna uwezekano akaishia kuchemsha.
“Chelsea inakaribia kumnunua mshambuliaji wa Colombia, Radamel Falcao, lakini kuna uwezekano mkubwa mshambuliaji huyu akafuata nyayo za Andriy Shevchenko na Fernando Torres. Washambuliaji hawa watatu waliwahi kuogopwa duniani wakiwa katika ubora wao, lakini kila mmoja wao aliumia goti na baada ya hapo hawajawahi kurudi tena katika ubora wao,” alisema Sharma.
“Chelsea ilimnunua Shevchenko kutoka AC Milan kwa Pauni 30 milioni mwaka 2006, baada ya kucheza Kombe la Dunia Ujerumani muda mchache tangu apone goti lake. Aliponunuliwa kwenda Stamford Bridge, alikuwa ameshapoteza makali yake,” alisema Sharma.
“Ni hivyo hivyo kwa Torres, lakini aliigharimu timu mara mbili zaidi na alicheza chini ya makocha na washambuliaji kadhaa kabla ya mkataba wake kukatishwa na kurudi Atletico akipitia AC Milan,” aliongeza Sharma.
“Na sasa inaonekana kuwa zamu ya Falcao kwenda Magharibi mwa London licha ya kufanikiwa kufunga mabao manne tu katika mechi 29 alizoichezea Manchester United msimu uliopita,” aliongeza mwandishi huyo.
Kauli ya Sharma inakuja siku chache tu baada ya Mourinho kudai kwamba ana uwezo wa kumrudisha Mcolombia huyo katika makali yake aliyokuwa nayo wakati akikipiga katika klabu za Porto na Atletico Madrid.
“Inaniumiza wakati watu England wanapoamini kuwa wamemwona Falcao halisi Manchester United. Ni mchezaji ninayemjua na nimemfuatilia tangu akiwa Atletico Madrid na kama nikiweza kumsaidia Falcao kurudi katika ubora wake nitafanya hivyo,” alisema Mourinho.
Mourinho anataka kumnunua mshambuliaji huyo kwa ajili ya kuziba pengo la mshambuliaji wake, Didier Drogba ambaye ametangaza kuondoka Stamford Bridge baada ya msimu ulioisha na Chelsea ikiwa bingwa.
“Tumempoteza mshambuliaji (Drogba) ambaye alifunga mabao manne katika Ligi Kuu, lakini mabao matatu kati ya hayo yalimaanisha pointi muhimu sana. Ni mshambuliaji ambaye alikuwa na uzoefu, ambaye kila dakika alikuwa bora kwetu, hata kwa dakika 10 za mwisho za kukaa na mpira, kupunguza munkari wa mechi,” alisema Mourinho.
“Kwa hiyo inabidi tununue mshambuliaji kwa sababu tunataka washambuliaji watatu wa kiwango kizuri,” aliongeza kocha huyo raia wa Ureno

0 comments:
Post a Comment