Aprili 7, 2012 pale nyota iliyong’ara katika tasnia ya filamu ilipozimika ghafla.
Steven Charles Kanumba alikuwa ni msanii, mwongozaji na mtayarishaji wa filamu aliyeifanya tasnia ya filamu nchini kuwa hai.
Kanumba, alikuwa ni zaidi ya mwigizaji kutokana na uwezo wake wa kutengeneza uhalisia wa kile alichokuwa akikifanya katika filamu.
Katika miaka yake ya mwanzo kaburini kila ilipofika Aprili 7 ya kila mwaka kulikuwa na tukio kubwa kwa ajili ya kumbukumbu yake.
Lakini mwaka huu hilo halikufanyika zaidi ya mama yake mzazi, Frola Mtegoa kwenda katika kaburi la msanii huyo akiwa na wasanii wachache wanaoliona pengo lake.
Wasanii hao na mama Kanumba waliambatana katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumkumbuka shujaa wao huyo aliyejijengea sifa kubwa Afrika Mashariki na kwingineko.
Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wetu, umebaini mambo yalitokea katika tasnia baada ya kifo cha Kanumba.
Moja ambalo lina athari kubwa ni kwa wale wasanii wote waliokuwa wakifanya kazi na marehemu kutengwa na watayarishaji.
Wengi wao hawashirikishwi katika filamu nyingine kulingana na kazi walizokuwa wakifanya kabla ya Kanumba kufariki dunia.
Ndani ya miaka mitatu wasanii hao waliokuwa wakimilikiwa na Kampuni ya Kanumba The Great Film hawana kazi kutokana kampuni hiyo kufa sababu kubwa ikiwa ni gharama za pango.
Kampuni imeshindwa kuzalisha filamu na aliyekuwa meneja wake Novatus Mayenja ‘Nova’ anakiri kuwa kifo cha bosi wake kimebadili kila kitu.
Nova amesema hali imekuwa mbaya, kwani hata wale watayarishaji waliokuwa wakiwahitaji hawawapi tena kazi na haelewi kuna uoga gani hadi imekuwa hivyo.

0 comments:
Post a Comment